|
Mwanaadamu yeyote, japo awe haamini kuwa yupo Mwenyezi Mungu na ipo siku moja viumbe wote tutakusanywa mbele yake, hawezi kuridhia kuona mwanawe anapata malezi mabaya kitabia, kiafya n.k. Kutoridhia pekee, hakuwezi kumpatia mwanawe malezi mema anayoyaridhia bila ya kufanya juhudi.
Moja ya juhudi za kufanikisha kuwa na watoto wenye tabia na afya njema, ni kuwapa Elimu ya Awali yenye mwelekeo sahihi inayotolewa na waalimu waliotayarishwa vyema kwa ajili ya kazi hiyo.
Hatua za utoaji wa Elimu ya Awali kwa mtoto
-
Mtoto hupewa Elimu ya Awali kabla ya mimba kutungwa kulingana na Itikadi na jamii ya Wazazi wake. Mfano Nabii Zakariya (a.s.) alipoomba kwa Allah (s.w.) apewe mtoto mwema, alisema"
"Mola, nipe kutoka kwako mtoto mwema, kwa hakika wewe ni Mwenye kusikia dua."
(Qur 3:38).
Pia Bwana wetu Muhammad (s.a.w.) ametufundisha kusoma dua kabla ya kufanya jimai mke na mume isemayo "Ewe Mwenyezi Mungu! Tuepushe na shari ya shetani (katika Ibada yetu hii), na umuepushe na shari ya shetani yule (mtoto) utakayeturuzuku (kutokana na ibada hii)."
Mtume (s.a.w.) akasema kwamba, kama atapatikana mtoto kwa tendo hilo, basi Allah (s.w.) atamlinda na kila aina ya shari ya shetani. Hii haina maana kwamba mtoto anayetungiwa mimba bila ya ile dua ya jimai, basi huwa muovu tangu siku ile walipojamiiana wazazi wake kwa kuwa hatopata Hifadhi ya Allah (s.w.) kujikinga na shetani muovu.
-
Mtoto hupewa Elimu ya Awali akiwa tumboni mwa mamaye. Mfano ni mama yake Maryam (Mke wa Mzee Imran) aliposoma kwenye uja uzito wake yafuatayo:
"Mola wangu! Kwa hakika mimi nimeweka nadhiri kwako, aliyetumboni mwangu awe wakfu; basi nikubalie dua yangu (nadhiri yangu). Bila shaka wewe ndiye usikiaye na ujuaye." (Qur 3:35) kinyume chake watu wabaya huomba kwa Allah (s.w.) kupata watoto, na wakishapata tu, huwakabidhi kwa vinyamkela, Sharif, n.k. ili wawalee na kuwalinda. Allah (s.w.) amesema:
"Yeye ndiye aliyekuumbeni katika nafsi moja; na akafanya katika (nafsi) hiyo wake zao, ili (kila mwanamume) apate utulivu kwake (mkewe). Na anapomuingilia hushika mimba (ambayo huwa) nyepesi kutembea nayo (yule mwanamke bila ya uzito).(Hata) anapokuwa mja mzito (mimba pevu inamtaabisha), wote wawili (mke na mume) huwa wanamuomba Mwenyezi Mungu, Mola wao (wakisema): "Kama ukitupa (mtoto) mwema (kamili), tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru. Basi anapowapa (mtoto) (Kiumbe) alichowapa. Lakini Mwenyezi Mungu ametukuka kuliko wale wanaowashirikisha naye." (Qur.7:189-190).
-
Mtoto hupewa Elimu ya Awali akiwa nyumbani kwa wazazi wake. Mfano ni Mzee Luqman ambaye Allah (s.w.) alimpa Hekima iliyompelekea kumlea mwanawe malezi mema; mzazi huyu alisema:
"...Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu, maana
shirki ndiyo dhuluma kubwa...
"Ewe mwanangu! Kwa hakika jambo lolote hata likiwa na uzito wa chembe ya hardali, likawa ndani ya jabali au mbinguni au katika ardhi, Mwenyezi Mungu atalileta (amlipe aliyelifanya); bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa mambo yaliyofichikana, (na) Mjuzi wa mambo yaliyodhahiri.
Ewe Mwanangu! Simamisha swala, na amrisha mema, na kataza mabaya, na uwe na subira juu ya yale yatakayokusibu; hakika hayo ni katika mambo yanayoazimiwa. Wala usiwafanyie watu kiburi (kwa kuwaangalia upande na kujitukuza), wala usitembee katika ardhi kwa maringo, hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila ajivunaye, ajifakharishaye. Na uishike mwendo wa kati na kati, na uteremshe sauti yako; kwa kinyume chake mtoto hujifunza tabia mbaya kwa mzazi wake kwa kutendewa kila atakalo ikiwa ni pamoja na kuangalia sinema za maasi n.k.
4. Mtoto hupewa Elimu ya Awali katika Kituo cha Malezi. Mfano Mke wa Mzee Imrani alipopata mtoto na kumpa jina Maryam, alimpeleka kwenye Kituo cha Malezi kwa Nabii Zakariya (a.s.) ambaye ndiye alikuwa Mwalimu pekee kwa wakati huo aliyetayarishwa na Allah (s.w.) kwa ajili hiyo. Nabii Zakariyya (a.s.) alitoa huduma kubwa ya malezi kwa Maryam na kila wakati alimzuru ili kulinda usalama wake. Allah (s.w.) amesema:-
"Basi Mola wake akampokea (yule mtoto mwanamke) kwa kubuli njema, na akamkuza kukua kwema, na akamfanya Zakariya awe Mlezi wake. Kila mara Zakariya alipoingia chumbani (kwake) alikuta nyakula mbele yake. Akasema: "Ewe Maryam! Unapata wapi hivi?" Akasema: "Hivi vinatoka kwa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hesabu." (Qur. 3:37).
Kinyume chake mtoto akipelekwa kwenye kituo cha malezi kilicho kinyume na Itikadi ya Kiislamu, au kwenye kituo ambacho walezi/Waalimu wake hawakutayarishwa vilivyo, mtoto atafunzwa Itikadi ya Kumkana Allah (s.w.) na kutokuwa na adabu. Hata akikutwa na vitu vya thamani hawezi kuhojiwa alikovipata kama alivyohoji Nabii Zakariya (a.s.), bali pengine na huyo Mlezi? Mwalimu ataomba apewe sehemu ya vitu hivyo, na huo ndiyo huwa mwanzo wa tabia mbaya za kutamani vya watu, kutokuwa na kinaa, na kuanza wizi, ujambazi na ukahaba.
Kazi ya kufundisha (ualimu)
Kufundisha ni moja ya kazi ngumu sana duniani, hasa kwa vile inahusika na malezi ya wanadamu hususan watoto. Tofauti iliyopo baina ya watoto, humfanya Mwalimu/Mlezi apambane na upinzani mkubwa katika shughuli zake za kufundisha.
Tofauti za watoto
Watoto hutofautiana kwa:-
|