|
KUUJUA Uislamu ni elimu na kila Muislamu anatakiwa aujue Uislamu wake. Kwa kweli muumini mjinga asiyejua dini anakuwa sawa na bendera inayofuata upepo.
Katika hadithi nyingi za Mtume (s.a.w.) muumini wa aina hii ametolewa kasoro nyingi.
Kwa sababu ya kuuelewa umuhimu wa elimu, Uislamu umehimiza Waislamu kuitafuta na kujifunza elimu
Mfumo wa maisha ya Muislamu umetawaliwa na sheria maalum ambapo ili mtu aishi kama Muislamu wa kweli inambidi awe na elimu.
Elimu huanza tangu utoto. Ni utaratibu uliopo tangu kutangaza kwa Uislamu kwa watoto wa Kiislamu kupelekwa katika madrasa kusoma elimu.
Hapo zamani wazazi walikuwa wakichukua jukumu la kuwasomesha wenyewe watoto wao ambapo kwa siku hizi hutegemea zaidi madrasah.
Kwa sababu hii miji yenye Waislamu wengi madrasah za watoto huonekana katika kila kona ya mji.
Uislamu haukubagui elimu itakayomletea manufaa binadamu katika dunia na akhera hivyo Uislamu haukuhimiza elimu ya dini tu bali hata ya dunia.
Kama wasemavyo wahenga kuwa elimu haina mwisho binadamu hujifunza kila siku hivyo Muislamu hujifunza elimu katika utoto na utu uzima kwa kadiri na kwa kiwango atakachoweza au kutosheka nacho.
Hata hivyo kiwango ambacho Muislamu anatakiwa afikirie ni kuijua misingi ya Uislamu wake kama vile nguzo za Uislamu na imani.
Jambo ambalo kwa kweli hivi sasa linasikitisha ni kwamba wazazi wengi wamesahau ule wajibu wao wa kuwapa elimu watoto wao.
Wazazi wengi huwahimiza watoto wao kwenda sahule ili kupata elimu ya dunia na kuisahau elimu ya dini.
Hii leo Waislamu tunakutwa na mitihani mingi kwa sababu ya kukosa elimu ya dini miongoni mwetu.
Vitendo vya Waislamu kushindwa kuutetea Uislamu wao pale inapolazimika na kufikia kudhalilishwa au kujifanyia mambo kinyume na misingi ya Uislamu ni matokeo ya ukosefu wa elimu ya dini.
Kwa muono wangu wazazi hawawahimizi watoto wao kwenda kusoma hasa pale wanapoonesha uvivu kama vile wanavyowahimiza kwenda skuli.
Mzazi anaridhika akimuona mtoto wake anaenda shule, lakini hamuulizi mbona hukwenda madrasah leo ama ikiwa amekwenda hamuulizi kama amesoma kitu gani na kama amefahamu ama ipo sehemu ambayo anahitajia msaada.
Jambo ambalo linawapa dhana watoto kuona kuwa skuli ni muhimu kuliko madrasah na hivyo kuendelea kukwepa masomo ya dini, na matokeo yake kunampelekea mtoto kuona masomo ya dini hayana faida yoyote.
Kila Muislamu ana wajibu mkubwa wa kuwaelimisha Waislamu kwamba elimu ni faradhi kwa Waislamu hivyo ni lazima watoto wa Kiislamu wahimizwe kusoma
|