English
Kuhusu Sisi
Malengo
Msaada
Fomu za Maombi
Darsah za Mwezi
Matangazo
Wasiliana Nasi
Wajibu wa Wazazi
Wajibu wa Wazazi
Madrasatunnur

Wazazi wote wawili wanahusika kwa ukamilifu na malezi haya. Malezi ya mtoto tunaweza kuyagawa katika sehemu mbili - Malezi ya kimwili na malezi ya kiroho.

Malezi ya kimwili ni yale yote anayofanyiwa mtoto ili akuwe katika afya njema. Malezi haya huanza mara tu mama anapoanza ujauzito. Baba ana wajibu wa kumtunza mkewe na kumpatia vyakula maalum ili mama na mtoto wake tumboni wawe na afya nzuri.

Jukumu la mama ni kufuata masharti ya kulea mimba anayopewa na Daktari. Baada ya mtoto kuzaliwa wajibu wa baba na mama kwa mtoto wao unabainishwa katika Qur'an:

"Na wanawake waliozaa wawanyonyeshe watoto wao miaka miwili kamili, kwa anayetaka kukamilisha kunyonyesha; na ni juu ya baba chakula chao (mama na mtoto wake) na nguo zao kwa sheria. Wala haikalifishwi nafsi yoyote ila kwa kadri ya wasaa wake."

"Mama asitiwe taabuni kwa ajili ya mtoto wake, wala baba (asitiwe taabuni) kwa ajili ya mtoto wake. Na juu ya mrithi ni kama hivyo. Na wote wawili wakitaka kumwachisha ziwa (kabla ya miaka miwili) kwa kuridhiana na kushauriana, basi si kosa juu yao. Na kama mkitaka kuwapatia watoto wenu mama wa kuwanyonyesha (wengine wasiokuwa mama zao) basi haitakuwa dhambi juu yenu kama mkitoa (kuwapa hao wanyonyeshaji) mlicho waahidi kwa sharia. Na mcheni Mwenyezi Mungu na jueni kwamba Mwenyezi Mungu anayaona yote mnayoyatenda. (2:233)."

Aya hii inatubainishia wazi kuwa hata katika umri wa kunyonya mtoto, wazazi wote wawili wanawajibika, kila mmoja katika nafasi yake. Katika kipindi chote cha kumlea mtoto jukumu kubwa la baba ni kuilisha familia, kuivisha na kuiweka katika makazi mazuri kwa kadiri ya wasaa wake.

Mama naye ana jukumu la kuwatunza watoto kwa kuhakikisha kuwa wanakula vilivyo, wanakuwa wasafi wa mwili na nguo na wanaishi katika mazingira masafi. Haya ndiyo malezi ya kimwili ambayo humuwezesha mtoto kuwa na afya mzuri na kukua vyema.

Malezi ya kimwili ni muhimu sana, lakini yenyewe tu hayatoshelezi kumuinua mtoto atakayekuwa raia mwema mwenye kuwajibika ipasavyo kwa wazazi wake na kwa jamii yake kwa ujumla. Uislamu haumtizami mwanaadamu kama mnyama, bali unamtazama kama Khalifa wa Mwenyezi Mungu (s.w.) ambaye asili yake ni mwili unaotokana na udongo na Roho takatifu, inayotokana na Mwenyezi Mungu (s.w.) kama tunavyojifunza katika Qur'an:

Na (kumbuka) Mola wako alipowaambia Malaika: "Hakika Mimi nitamuumba mtu kwa udongo mkavu unaotoa sauti, wenye kutokana na matope meusi yaliyovunda! Basi nitakapo mkamilisha na kumpulizia roho inayotokana na Mimi, basi muangukieni kwa kumtii"(15:28-29).

Kutokana na aya hizi tunajifunza kuwa kilichomfanya mwanaadamu kuwa na hadhi juu ya viumbe vyote hata malaika ambao waliamrishwa na Mwenyezi Mungu (s.w.) kumuangukia kwa utii, si uzuri wa sura yake au umbile lake, bali ni ile Roho takatifu inayotokana na Mwenyezi Mungu (s.w.). Lakini si kila mwanaadamu atakaye stahiki heshima hii ya kuangukiwa kwa utii na malaika. Anayestahiki heshima hii ni yule tu atakayeishi kwa kufuata tabia na mwenendo anaoridhia Mwenyezi Mungu (s.w.) au kwa kufuata maadili mema anayoyaridhia Mwenyezi Mungu (s.w.).

Atakayeishi kwa kufuata msukumo wa matashi ya mwili (unyama) wake na kuukataa mwongozo wa Mwenyezi Mungu (s.w.), hadhi yake itashuka na kuwa duni kuliko vilivyo duni kama Mwenyezi Mungu (s.w.) anavyhotufahamisha:

Bila shaka tumemuumba mwanaadamu kwa umbo lililo bora kabisa. Halafu tukamrudisha chini kuliko walio chini. Ila wale wenye kuamini na kutenda mema, watakuwa na ujira usio kwisha. (95:4-6).

Hivyo, wazazi pamoja na kuwalea watoto wao kimwili, hawana budi kuhakikisha kuwa wanawalea kimaadili kwa kuwafunza tabia na mwenendo mwema anaoridhia Mwenyezi Mungu (s.w.). Mtoto aanze kufunzwa tabia ya Kiislamu tangu mwanzo, hasa pale anapoanza kuongea na kuelewa lile analoelekezwa.

Mtoto afikapo umri wa miaka mitano, ahudhurishwe pamoja na watoto wenzake katika kituo cha malezi ya watoto (madrasah) ambapo watoto wanalelewa Kiislamu.

Wazazi wa kiislamu hawana budi kujumuika pamoja katika mtaa wao na kuhakikisha kuwa panakuwa na madrasah yenye utaratibu mzuri wa kufundisha watoto Uislamu na kuwalea katika mwenendo na tabia ya Kiislamu, tangu wanapokuwa na umri wa miaka mitano mpaka kufikia umri wa miaka 15.

Mzazi ahakikishe kuwa watoto wa umri wa miaka saba na kuendelea wanatekeleza ipasavyo ibada maalum kama vile swala, swaumu, na kadhalika.

Watoto wa umri wa miaka 10 na kuendelea ni lazima watekeleze maamrisho yote ya Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa kadiri ya uwezo wao. Wakiacha makusudi kufanya hivyo wazazi au walezi wao wawaadhibu. Pia mzazi anatakiwa ampeleke mtoto wake shuleni anapofikia umri wa kwenda shule na kufuatilia masomo yake ili kumuandaa mwanawe kuwa raia hodari atakayeweza kutoa mchango wake katika kuiendeleza jamii kwa kadiri ya ujuzi wake.

Huu ndio utaratibu unaosisitizwa na uislamu katika kumlea mtoto ili ainukie katika Dini ya Uislamu, ambayo ndio Dini yake ya asili kama tunavyojifunza katika hadithi ifuatayo:

Abu Hurairah amesimulia kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu amesema: "Hapana mtoto asiyezaliwa katika (dini ya) asili (Uislamu). Kisha wazazi wake humfanya kuwa Myahudi au Mkristo au Mmajusi. Kisha akasema: "Umbile la Asili ndilo umbile Mwenyezi Mungu aliloumbia watu. Hakuna mabadiliko katika maumbile ya viumbe vyote vya Mwenyezi Mungu". (30:30) - (Bukhari na Muslim).

Hadithi hii iliyomalizia na aya ya Qur'an (30:30) inatukumbusha kuwa Uislamu ndio dini inayolingana na umbile la mwanaadamu na kwa hiyo kila mtoto huzaliwa Muislamu. Hivyo ni wajibu wa kila mzazi Muislamu kumlea mtoto wake katika dini yake ya asili kwa jitihada zake zote mpaka amfikishe kwenye utu-uzima wake. Hapana shaka kutekeleza wajibu huu wa kuwalea watoto wetu katika maadili ya Kiislamu ni jambo gumu linalohitajia msaada wa Mwenyezi Mungu (s.w.). Muumini wa kweli pamoja na jitihada zake katika kutekeleza wajibu huu hana budi kuomba msaada wa Mwenyezi Mungu (s.w.) kwa dua ambayo Yeye mwenyewe ametufundisha katika Qur'an:

Mola wetu! Tupe katika wake zetu na watoto wetu yaburudishayo macho (yetu) (nyoyo zetu), na utujaalie kuwa waongozi wa wamchao (Mungu). (25:74).

Ee Mola wangu! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu, na niwezeshe nifanye vitendo vizuri unavyovipenda, na unitengenezee watoto wangu; kwa yakini ninatubu kwako; na hakika mimi ni miongoni mwa waliosilimu (walionyenyekea). (46:15).

Watoto wetu wanapokuwa wakubwa tuwaozeshe mapema kwa wanaume au wanawake wenye mwenendo na tabia ya Kiislamu na daima tusiache kuwapa nasaha njema. Hebu turejee Qur'an tuone nasaha ya Luqman kwa mwanawe:

Na (wakumbushe) Luqman alipomwambia mwanawe; na hali ya kuwa anampa nasaha. Ewe mwanangu! Usimshirikishe Mwenyezi Mungu, maana kushirikisha ndiyo dhulma kubwa.

Ewe mwanagu! Kwa hakika jambo lolote lijapokuwa na uzito wa chembe ya hardali, likawa ndani ya jabali au mbinguni, au katika ardhi, Mwenyezi Mungu atalileta (ampe anayehusika) bila shaka Mwenyezi Mungu ni Latifu (Mpole), Mjuzi wa kila jambo.

Ewe Mwanangu! Simamisha swala, na uamrishe mema, na ukataze mabaya, na usubiri juu ya yale yatakayokusibu. Hakika hayo ni katika mambo yanayostahiki kuazimiwa. Wala usiwatazame (watu kwa jeuri) kwa upande mmoja wa uso, wala usiende katika ardhi kwa maringo; hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila ajivunae, ajifaharishaye.

Na ushike mwenendo wa katikati, na uteremshe sauti yako, bila shaka sauti ya punda ni mbaya kuliko sauti zote (mbele ya Mwenyezi Mungu s.w.).

Jambo jengine muhimu kwa wazazi katika kuwalea watoto wao ni kuwa na upendo na huruma juu yao. Ukali wa kupindukia na ukaripiaji wa mara kwa mara watoto si malezi mazuri na kamwe mtoto haleleki vyema katika mazingira kama hayo, Mtume (s.a.w.) aliye kiigizo chetu pekee, alikuwa ni mlezi mwema mno. Alikuwa na huruma na upendo mkubwa mno kwa watoto wake na wajukuu zake kama tunavyojifunza katika hadithi zifuatazo:

Aysha (r.a.) amesimulia: Sijamuona mtu aliyeshabihiana kitabia na mwenendo na Mtume (s.a.w.) kuliko Fatma. Alipokuja kwa Mtume, Mtume (s.a.w.) alimsimamia, kisha alimchukua kwa mkono wake na kumbusu na kisha kumkalisha karibu yake. Na Mtume (s.a.w.) alipokwenda kwake, Fatma alikuwa akimsimamia, kisha akimtwaa kwa mkono wake na kumbusu, na kumkalisha karibu naye. (Abu Daud).

Pia Mtume (s.a.w.) amesisitiza kuwapenda na kuwahurumia watoto kwa kuwabusu kama hadithi zifuatazo zinavyotufahamisha:

Abu Hurairah ameeleza kuwa Mtume wa mwenyezi Mungu alimbusu mjukuu wake, Hassan bin Ali, mbele ya Aqra bin Habis ambaye alisema: Nina watoto kumi na sijambusu hata mmoja wao. Mtume wa Mwenyezi Mungu alimwangalia na kusema: "Yule asiye na huruma hatahurumiwa". (Bukhari na Muslim).

Aysha (r.a.) ameeleza kuwa Mwarabu wa jangwani (Bedui) alikuja kwa Mtume (s.a.w.), akasema: Nini! Unabusu watoto? Sisi hatuwabusu. Mtume (s.a.w.) akasema: "Sina la kuwasaidia, kwani Mwenyezi Mungu (s.w.) ameondoa huruma nyoyoni mwenu". (Bukhari na Muslim).

Hadithi hizi mbili zinatusisitiza tuwalee watoto wetu kwa huruma na upendo. Kuwabusu watoto ni kielelezo cha upendo wetu kwao.

Pamoja na kuwalea watoto wetu ipasavyo, hatuna budi kuchunga mipaka ya Mwenyezi Mungu (s.w.) katika kufanya kazi hiyo. Huruma na upendo kwa watoto wetu kamwe kusitupelekee kwenda kinyume na maamrisho ya Mwenyezi Mungu (s.w.) na Mtume wake.

Muislamu anatakiwa ampende Mwenyezi Mungu (s.w.) na Mtume wake kuliko hata anavyoipenda nafsi yake, sembuse nafsi nyingine. Mara nyingine, baadhi ya wazazi, kwa ajili ya kuwapenda na kuwahurumia watoto wao, huwaachia huru kwenda kinyume na maamrisho na makatazo ya Mwenyezi Mungu (s.w.) ili kuwaridhisha watoto wao hili ni kinyume na mafundisho ya Mtume (s.a.w).

Aidha Katika harakati za kuchuma mali husahau jukumu la kuwalea watoto wao.Kuhusu jambo hili Waislamu hawana budi kila mara kukumbuka nasaha ya Mwenyezi Mungu (s.w.) katika aya zifuatazo:

Enyi mlioamini! Yasikusahaulisheni mali yenu wala watoto wenu kumkumbuka Mwenyezi Mungu! Na wafanyayo hayo, hao ndio wenye kuhasirika. (63:9).

Enyi mlioamini! Kwa yakini baadhi ya wake zenu na watoto wenu ni maadui zenu, basi jihadharini nao... (64:14).

Bila shaka mali zenu na watoto wenu ni mtihani. Na kwa Mwenyezi Mungu kuna ujira mkubwa kabisa. (64:15).

Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia. Na vitendo vizuri vibakiavyo ndivyo bora mbele ya Mola wako kwa malipo na tumaini bora. (18:46).

Aya hizi kwa ujumla zinatukumbusha kuwa pamoja na kuwapenda na kuwahurumia wake zetu na watoto wetu na pamoja na kuipenda mali na vyote vingine vinavyopendeka, hatuna budi kuhakikisha kuwa upendo wetu juu ya Mwenyezi Mungu (s.w.) na Mtume wake unakuwa juu ya kitu chochote kile kama Mwenyezi Mungu (s.w.) anavyotutanabahisha tena katika aya zifuatazo:

Enyi mlioamini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa vipenzi (vyenu) ikiwa wanastahabu (wanapenda) ukafiri kuliko Uislamu. Na katika nyinyi atakayewafanya hao kuwa ndio vipenzi vyake, basi hao ndio madhalimu.

Sema: Kama baba zenu na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa zenu na mali mlizochuma, na biashara mnazoogopa kuharibikiwa, na majumba mnayoyapenda, ni vipe yake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu maasi. (9:23-24).

Jambo lingine muhimu la kuzingatia zaidi katika kuwalea watoto ni kutokuwa na upendeleo au ubaguzi kati ya watoto. Wazazi wanawajibika sawa kwa watoto wao wote na kila mtoto anahaki sawa na mwingine katika kupendwa na kuhurumiwa na wazazi wake

Madrasatunnur Educational Trust